IMANI HENRICK LUVANGA: SHUJAA WA KIZAZI CHA SASA, MWANGA WA VIJANA NA NGUZO YA NDOTO ZILIZOAMKA



IMANI HENRICK LUVANGA: SHUJAA WA KIZAZI CHA SASA, MWANGA WA VIJANA NA NGUZO YA NDOTO ZILIZOAMKA

Imani Henrick Luvanga ni mwanahabari wa Tanzania, mbobezi wa maudhui ya kidijitali, na mtetezi wa haki za kidijitali ambaye amejijengea nafasi muhimu katika tasnia ya habari na uwajibikaji wa kijamii. Akiwa na msingi wa kitaaluma katika uandishi wa habari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Imani ameendelea kuwa sauti inayoheshimika na mfano wa kuigwa kwa vijana wengi nchini.

Safari yake ya taaluma ilianza kwa ndoto ya kuwa mwanasheria alipokuwa sekondari. Hata hivyo, alipofika UDSM alitambulika kwa uwezo wake wa kuwasiliana, kuzungumza hadharani, na kuelezea masuala kwa umahiri. Hapo ndipo alibadilisha mwelekeo na kuikumbatia taaluma ya uandishi wa habari kwa moyo wote. Akiwa chuoni, alijiunga na Shule Kuu ya Uandishi na Mawasiliano kwa Umma mwaka 2019, na katika kipindi hicho akapokea mafunzo maalum kupitia Nukta Africa kuhusu uandishi wa habari unaozingatia takwimu, nishati ya maendeleo, na utengenezwaji wa maudhui ya hadithi kwa njia mbalimbali (multimedia storytelling). Mafunzo hayo yalijenga msingi imara wa umahiri wake wa baadaye katika tasnia.

Baada ya zaidi ya miaka mitano ya uzoefu, Imani ameibuka kuwa mmoja wa wanahabari vijana wanaoaminika na wanaotambulika kwa ubunifu na uthubutu. Akiwa na umri wa miaka 25 tu, alipata nafasi ya kuwa Mkuu wa Kituo cha Kings FM Radio, hatua ambayo ni nadra na ya kipekee katika sekta ya habari kwa mtu mwenye umri mdogo. Chini ya uongozi wake, kituo hicho kilipitia mageuzi makubwa na kikawa miongoni mwa vituo vyenye mwelekeo wa kisasa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa sasa Imani anafanya kazi na Crown Media Tanzania kama Programmes Manager wa Crown TV, huku pia akitumia uwezo wake kama mwanahabari wa multimedia. Katika nafasi hiyo, anahusika na usimamizi wa maudhui, uratibu wa vipindi, na uundaji wa mikakati yenye lengo la kuifikia jamii kwa njia pana zaidi. Mbali na majukumu hayo, yeye ni mwanzilishi mwenza wa Mwanga Hub, taasisi inayolenga kuwawezesha vijana, wanawake, na makundi yaliyoko pembezoni kwa kuwapa elimu ya haki za kidijitali, usalama wa mtandaoni, na uandishi wa habari.

Kupitia kazi zake, Imani amekuwa mstari wa mbele kuibua mijadala kuhusu haki za mtandaoni, usawa, uwakilishi, na ukatili wa kijinsia unaofanyika kupitia majukwaa ya kidijitali. Haya ndiyo yanayompa msukumo wa kuendesha podcast yake iitwayo Dig It With Imani, ambako anazungumza kuhusu masuala haya kwa kina na kuwapa nafasi wale ambao mara nyingi hawapati jukwaa. Umahiri wake, uelewa mpana, na ujasiri wake wa kukabiliana na changamoto za kijamii vimemfanya kuwa mkufunzi aliyesajiliwa na DW Akademie na mshirika wa mashirika ya kimataifa kama Thomson Reuters Foundation kupitia mradi wa “Digital Rights as Human Rights.”

Katika muktadha mpana, Imani anachukuliwa kama mfano wa kizazi kipya kinachojituma, kinachoamini katika mabadiliko, na kinachotumia taaluma ya habari kuleta athari chanya. Ameonyesha kuwa umri si kizuizi cha kuleta mapinduzi, na kwamba uthabiti, maarifa, na maadili vinaweza kumfanya kijana yeyote kuwa chanzo cha mwanga katika jamii. Kupitia kazi zake zote kuanzia uandishi, mafunzo, uongozi wa media, hadi utetezi wa haki amekuwa kiungo muhimu kati ya vijana na uchangamfu wa dunia ya teknolojia na uwajibikaji wa kijamii.

Kuna watu wanaopita duniani wakiwa kimya, lakini miguu yao inabeba historia nzima ya vizazi. Kuna watu hawapigi kelele, lakini matendo yao yanalia kwa nguvu kama baragumu la matumaini. Watu wanaogeuza ndoto za wengine kuwa ukweli. Miongoni mwao, Tanzania imembariki mmoja  Imani Henrick Luvanga. Katika ulimwengu wa habari na haki za kidijitali, jina la Imani limekuwa kama mwanga unaovunja giza, mlima unaosimama thabiti katikati ya dhoruba za kijamii, na njia inayokatiza pori gumu la changamoto kwa vijana wengi wanaoota kuwa wanahabari, watangazaji, au watetezi wa jamii.

Safari ya Imani ilianza kwa unyenyekevu akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mahali ambapo ndoto yake ilikomaa na kuona mwanga wake wa kwanza. Kutoka mwanafunzi wa uandishi hadi kuwa mwandishi, mtangazaji, mkufunzi wa haki za kidijitali, kiongozi wa vipindi na mratibu wa programu  safari yake ni ushuhuda kuwa msingi madhubuti huzaa matunda yasiyoisha. Lakini hadithi yake haiishii kwenye vyeti; inaishi kwenye watu. Kwa miaka kadhaa, amekuwa mlezi wa vipaji, mwalimu wa kijamii, mwangaza wa wavulana na wasichana waliopoteza dira, na nguzo ya vijana wanaopigania nafasi kwenye vyombo vya habari. Kupitia kazi zake, amesimama kama daraja kati ya kizazi kipya na fursa zilizofichika. Amefundisha, amehamasisha, ameinua, na muhimu zaidi amewapa vijana imani kuwa wanaweza.

Jina lake “Imani” limekuwa neno la kutia nguvu kwa wengi. Si kwa sababu tu anafanya kazi, bali kwa jinsi anavyogusa maisha. Amewainua walioanguka. Amefungua milango kwa waliokata tamaa. Ameamini kwenye vipaji ambavyo wengine hawakuona. Amewaongoza wale walioogopa kuanza. Na miongoni mwa vijana aliowainua, mmoja amesimama kama ushuhuda hai kijana ambaye leo hii jina lake linang’aa katika anga la utangazaji Tanzania.

Seleman Joseph Bundala : anayejulikana kama Kilimboka  ni mfano halisi wa kile ambacho Imani Henrick anaweza kufanya katika maisha ya kijana. Leo hii Kilimboka ni mtangazaji wa kituo kikubwa na cha heshima sana cha A FM 92.9 Dodoma, kupitia vipindi maarufu vya Kijiweni na Love Vibes, mbali na kufanya kazi pia na Kings fm (wakati huo meneja wake alikuwa ni Imani Enrick Luvanga) na  Global TV. Lakini safari yake ina mizizi marefu kuliko wengi wanavyoifahamu. Kuna kauli moja ya Kilimboka ambayo imekuwa kivuli cha simulizi hii nzima, kauli inayobeba uzito wa shukrani, maumivu ya safari na furaha ya kutimiza hatua.

“Huenda bila Imani Henrick basi mimi nisingekuwa hapa. Ameniinua, amenisaidia sana. ila, Naweza kusema yeye ndiye mlango wa mimi kufikia hapa. Sijasema nimefanikiwa sana, lakini nimepiga hatua kubwa. Leo nimefanya kazi na Kings fm, Global TV na sasa nipo A FM Radio kwa sababu yake. Na bado naendelea kuziishi nyayo zake. Sitaacha kumfuatilia. Nampenda sana boss wangu.”

Huu siyo msisimko wa maneno  ni historia. Ni ushuhuda. Ni dira kwa vijana wengine wanaopambana. Kilimboka ni moja ya mazao ya juhudi za Imani, kijana aliyepata jukwaa kupitia moyo wa kiongozi aliyekuwa tayari kusukuma wengine mbele bila wivu, bila mashindano, na bila kuchoka. Hadithi yake imesimama kama kioo cha kuonesha kuwa Imani anaweza kuibua almasi kwenye mawe ambayo dunia ilidhani hayana thamani.

Kupitia mafunzo, uandishi, mitandao ya haki za kidijitali na uongozi wake kwenye media, Imani ameunda mazingira mapya kwa vijana. Amejenga ujasiri kwao kuzungumza. Amefundisha jinsi ya kutumia kalamu kama silaha ya maarifa, na kamera kama darubini ya jamii. Amesimama kupinga ukatili wa mtandaoni na kulinda sauti za walio kimya. Ameinua wanawake, vijana, na wale ambao jamii ilikuwa imewanyima nafasi. Alipoanzisha Mwanga Hub, alileta maana halisi ya jina lake  kuwa mwanga kwa waliopotea, na dira kwa wanaotafuta njia.

Imani si mwanasiasa, si mwanajeshi, wala si mtu wa makundi makubwa  lakini ni shujaa wa amani, anayepigana vita vya fikra, usawa, elimu na maadili kwa kutumia kalamu na sauti. Katika taifa ambalo vijana wanahitaji miwani ya kuona mbali, Imani amekuwa kama taa ya kuelekeza njia  bila yenyewe kuhitaji kushangiliwa. Ni shujaa anayefanya mapinduzi kimya, lakini matokeo yake yanatikisa anga ya taifa.

Hadithi ya Imani Henrick Luvanga haijafika mwisho. Inazidi kuandikwa  si kwa mkono wake tu, bali kwa mikono ya vijana wote aliowagusa. Kilimboka ni mfano mmoja tu, lakini si wa mwisho. Kwa kizazi cha leo, Imani si tu mtu  ni dira bali Ni wito wa kupanda milima bila kuogopa. Ni ushuhuda kwamba mtu mmoja anaweza kubadilisha vizazi vitatu. Na kwa Tanzania, kwa vijana, kwa media, kwa jamii  Imani Henrick Luvanga ni zawadi isiyojirudia mara mbili.

Maoni

Mashairi Pendwa Zaidi

Ushairi : Maumivu

Shairi: Kipenzi changu

Shairi: Moyo Wa Subira